top of page

Kibibi's Story

This story and photography is part of the exhibition Ethical Storytelling: Feelings and Memories.

#EthicalStorytellingExhibit

thumbnail_Kibibi.jpg

Untitled Story - Kibibi

Kwa majina naitwa Mwanaisha. Mwanaisha ni mama aliyezaliwa mwaka wa 1987 katika Kijiji kinachoitwa Mwandoni. Nilisoma hadi darasa la nane japo Mwenyezi Mungu hakunijalia kwenda katika shule ya upili. Hapo ndipo nilipoanza kufanya biashara ndogo ndogo kama vile kuuza mahamri na kadhalika.Maisha yaliendelea vizuri kwani nilipata kila siku riziki yangu.

Katika safari ya maisha yangu nilipatana na kijana ambae tulipendana sana.Tulifikia katika hali ya ndoa.Hapo ndipo nilipoanza maisha yangu ya ndoa. Baada ya muda nilibeba ujauzito nikajifungua mtoto wa kike. Kwasababu  ya malezi ya mtoto wangu sikuendelea  na biashara.

Mimi na mavyaa hatukuelewana. Siku moja ya ijumaa tulielekea msikitini mimi, bwanangu na mtoto wetu.Tulipokuwa  tukitoka, mavyaa alituona na kutuita. Alituambia ni lazima twende hospitalini tukaone mtoto wa nduguye aliyekuwa mgonjwa na alikuwa amelazwa. Mume wangu alimwambia hakuwa na shida na mtoto lakini alikuwa haelewani na nduguye. Mavyaa hakutaka kuelewa ivo tulielekea hospitalini. Mume wangu hakuelewana na mama yake ,waligombana hadi wakafika hospitalini. 

Tulipofika mimi sikuingia ndani kwasababu hatukusikizana kabisa na familia hiyo. 

"Huyu mtoto wenu hawezi gonjeka na kulazwa mahali kama hapa na akose kufaulu", mavyaa aliyazungumza  maneno hayo. Maneno hayo yaliniumiza sana. Baada ya kumuona mtoto tulirudi nyumbani na maisha yakaendelea.

Usiku wa siku hiyo mtoto wangu aligonjeka. Alianza kuwa mwili moto na kuharisha. Asubuhi yake bwanangu alienda kazini. Mchana ulipofika mtoto wangu alizidiwa, joto la mwili likazidi kuwa juu. Nilimchukua na kumpeleka hospitalini.

Daktari alimdunga sindano na kumueka "drip". Baada ya muda kidogo kupita, daktari alinipa barua ya kuniruhusu nimpeleke hospitali kuu ya Mombasa inayoitwa Makadara. Kwasababu hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Nilipofika, mtoto wangu alilazwa hadi asubuhi. Niliingia ili kumwangalia mtoto wangu. Nilimwona akitoa mapovu kwenye mdomo wake. Nilimwita daktari ili aje amwangalie. Alipofika alimtazama mtoto na kuniambia kwamba mtoto wangu ameaga dunia. Niliumia sana kwani alikiwa mtoto wangu pekee. Tulikaa na familia yangu na kujadili kuhusu mazishi. Jioni ya Siku hiyo mwanangu alizikwa.

 

Baada ya miezi sita niliubeba ujauzito mwengine. Maisha yaliendelea Kama kawaida. Nilirudi katika kufanya biashara yangu tena. Nilipokuwa kwenye biashara yangu nilimwona mavyaa, alinitazama kwa macho ya ukali hadi mwili wangu kusisimkwa. Nilishindwa na la kufanya. Hivo nikaupoteza ujauzito wangu. Hapo ndipo nilipoapa kutoshika mimba tena. Nilimweleza bwanangu na kumwambia aowe bibi mwengine. Kwani nilikuwa nimechoshwa na tabia za mavyaa.

Nilienda kwa muumini wa dini yangu ya kiislamu na kumweleza . Aliniambia kwamba atakuja nyumbani ili kunisomea. Nilimweleza bwanangu ivo naye akamweleza mama yake. Alipoelezwa hivo alianza kuteta. Alikesha kuteta. 

Siku iliyofwata muumini alikuja na mavyaa hakuwa na budi ila kukaa na kusikiza kisomo. Baada ya Siku kadhaa mavyaa alibadilika kabisa na akawa mtu mzuri, mwenye kujali maslahi ya watu wengine. Japo nilimwogopa kidogo. Sikuamini macho yangu. 

Baada ya miezi nane nilibeba mimba nyengine. Mwenyezi Mungu alinisaidia katika safari ya ujauzito wangu. Ilipofika siku ya kujifungua nilijifungua salama. Maisha yaliendelea vizuri sana. Mtoto wangu alikuwa vizuri bila shida yoyote hivyo nikamzalia mwenzake.

Baba Yao alisafiri na kwenda Nairobi kwasababu ya kazi yake.Tuliwasiliana kwa simu. Alitimiza mahitaji yake kama baba ya watoto kwa muda.Mara akaanza kubadilika, akawa hashiki simu zangu na wala hajibu meseji zangu.

Siku moja nilimpigia na simu ikashikwa na mwanamke . Akaniambia niachane na mume wake na niache kumsumbua. Sikuwa na la kufanya. Nilijikaza moyo na kusema maisha yaendelee. 

Asubuhi moja nikiwa na watoto wangu tuliskia mlango ukibishwa. Nilienda kufungua na kumpata bwana yangu hapo,sikuamini macho yangu. Nilimkaribisha ndani. Alianza kulia na kuniomba msamaha. Sikuwa na la kufanya ila kumsamehe  kwani alikuwa mzazi mwenzangu.

 

Afya yake ilikuwa imedhoofika sana na alikuwa mgonjwa. Nilimpeleka hospitali na kupata dawa. Nilimtunza sana ila siku ilifika nae akaaga dunia kwa sababu ya ugonjwa ulioitwa "kidney stones". 

Mama yake aliposikia hivo alikuja kumwona alipokuwa mgonjwa hospitalini ilhali siku ya mazishi hakuja. Nilimzika bwanangu. Ndugu na marafiki walinisaidia katika mchango. 

Siku moja nilipokea simu kutoka kwa chifu wa mtaa wa mavyaa ambao alikuwa akiishi. Aliniambia kwamba nilimuuwa bwanangu hivyo mali aliokuwa ameacha bwanangu singeweza kupata. Nilishtuka sana kwani ningewezaje kumuuwa mume wangu ilhali mimi ndie niliye mtibu hadi siku zake kufika.

Aliniambia singeweza kupata hizo mali. Nilikwambia kwamba ni sawa. Sikuwa na la kufanya ila kuendelea na maisha yangu na kuwalea watoto wangu. Hadi sasa wasichana wangu ni wakubwa na wanaendelea masomo. Mmoja yuko kidato cha pili na mwengine darasa la saba. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwani yeye ndiye hupeana na kuchukuwa. Kila kitu hufanyika kwa ajili ya Allah.

​

bottom of page